TANZANIA

Tanzania na Burundi zimesaini makubaliano kuhusu Mkongo wa Mawasiliano

FEBRUARI 23, 2024
Border
news image

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Mhe. Nape Nnauye pamoja na viongozi na wadau wa mawasiliano, wameshuhudia utiaji saini mkataba wa makubaliano ya kibiashara kati ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Burundi Backbone System (BBS) katika hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo, Waziri Nape amesema tukio hilo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiteknolojia kati ya Tanzania na Burundi, na kufungua njia ya ushirikiano mpana zaidi katika sekta ya mawasiliano. Mkataba huo mpya wa kibiashara kati ya TTCL na BBS una thamani ya dola za Kimarekani Milioni 3.3, sawa na Shilingi za Kitanzania Bilioni 8.3.

Waziri Nape amebainisha kuwa matokeo mazuri ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano yamepelekea Serikali ya Burundi, kupitia BBS, kukubali kuongeza huduma hizo. Mkataba huo utaimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Burundi na kuboresha mawasiliano kati ya nchi hizo mbili.

Waziri Nape amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake thabiti ya kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ya kimkakati kama njia ya kufanikisha maendeleo ya nchi. Malengo ya Serikali ni kufikia mwaka 2025, Mkongo wa Taifa ufikie kilometa 15,000 na kuunganisha mikoa na wilaya zote.

Waziri Nape ametoa rai kwa TTCL kuhakikisha kuwa BBS inapata huduma bora na yenye uhakika kulingana na mkataba uliosainiwa. Hii ni muhimu kwa sababu BBS inategemea huduma za TTCL kuendesha shughuli zake kwa ufanisi.

Katika mkutano huo, Waziri Nape pia amewaomba Burundi kutumia Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) kilichopo Tanzania. Kituo hicho ni miongoni mwa vituo bora barani Afrika, kinachotumia teknolojia za kisasa, na kina usalama wa kutosha. Waziri Nape ameongeza kuwa kituo hicho kina wafanyakazi wenye ujuzi wa kukisimamia na kukiendesha.

Mkataba huo wa ushirikiano umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga, na Mkurugenzi Mkuu wa BBS, Bw. Jeremie Diomede Hageringwe.

MTV Tanzania